Ijumaa, 25 Aprili 2025

Vijana 10 wa Kimashale Wapambana na Umaskini kwa Ubunifu wa Uchomeleaji Vyuma

Gairo, Morogoro – Katika kijiji kidogo cha Kimashale, kata ya Chakwale wilayani Gairo, vijana 10 wameandika historia mpya ya matumaini, wakichukua hatua ya kishujaa kupambana na adui mkubwa wa maendeleo – umaskini. Kwa mtaji wa Shilingi milioni 3 tu, walizindua rasmi shughuli za uchomeleaji vyuma mwezi Machi 2023, wakiongozwa na ndoto, juhudi, mshikamano na maono ya kuona mabadiliko katika jamii yao.

Kupitia uhitaji mkubwa wa huduma ya uchomeleaji katika kijiji chao na maeneo ya jirani, kikundi hiki kilitambua fursa ya kipekee na kuichangamkia kwa ubunifu. Kwa kuonesha uwajibikaji, weledi na mipango thabiti ya biashara, walifuzu kupata mkopo wa Shilingi milioni 15 kupitia asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri – fedha maalum zinazotolewa kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu – kwa riba nafuu ya asilimia 4 tu.

Mafanikio yao hayakuchelewa kuonekana. Kupitia mkopo huo, walinunua vifaa vya kisasa vya uchomeleaji ambavyo vimeongeza tija na ufanisi wa kazi zao. Ubora wa bidhaa uliongezeka, hali iliyowavutia wateja kutoka vijiji vya jirani na kuimarisha soko lao. Kwa sasa, si tu kwamba wanapata kipato kizuri, bali pia wamezalisha ajira kwa vijana wengine wa kijijini, na hivyo kuchochea uchumi wa Kimashale.

Mfano huu unathibitisha kwa vitendo kwamba maendeleo si ndoto au zawadi ya bahati, bali ni zao la mipango madhubuti, ushirikiano wa kijamii na uwekezaji sahihi. Vijana wa Kimashale ni mfano halisi wa nguvu ya kizazi kipya chenye ari ya kubadili maisha na kuchangia ustawi wa taifa.

Tuwape nafasi vijana. Tuwasilikize. Tuwavunie uwezo wao. Tuwasaidie kugeuza mawazo kuwa miradi yenye tija. Kwa pamoja, tunaweza kuijenga Tanzania yenye uchumi shindani kwa kutumia rasilimali yetu muhimu zaidi vijana.

Alhamisi, 24 Aprili 2025

VIJANA WA KILOSA WANG’ARA KUPITIA KILIMO CHA ALIZETI – MVIHAWIKI YAWAINUA KIUCHUMI

Vijana 40 kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa wameungana kupitia Mtandao wa Vijana wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa (MVIHAWIKI) kuanzisha shamba la alizeti lenye jumla ya ekari 20, ikiwa ni sehemu ya mpango wa kuwawezesha kiuchumi. Kati ya vijana hao, 29 ni wanaume na 11 ni wanawake.

Maandalizi ya shamba hilo yamegharimu shilingi milioni 3.72 zilizotolewa kupitia mapato ya ndani ya halmashauri hiyo, chini ya Mpango wa Maendeleo ya Vijana wa Taifa wa mwaka 2007 na Mkakati wa utekelezaji wa miaka 10 (2024–2034).

Mradi huu unaunga mkono maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kupitia program ya Build a Better Tomorrow (BBT), inayolenga kuwainua vijana kiuchumi kupitia sekta ya kilimo.

Jumanne, 18 Machi 2025

JE, KAULI MBIU YA MHE. RAIS, DKT. SAMIA SULUHU HASSAN – 'KAZI NA UTU TUNASONGA MBELE' INA MAANA GANI KWA MAENDELEO YA TANZANIA?


Kauli mbiu ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan –"Kazi na Utu Tunasonga Mbele" – ni dira ya maendeleo inayobeba dhana ya uwiano kati ya maendeleo ya kiuchumi na maadili ya kijamii. Kauli hii inaonesha dhamira ya serikali ya awamu ya sita katika kuhakikisha Tanzania inapiga hatua za kimaendeleo kwa kudumisha utu, mshikamano na utamaduni wa Kitanzania. 

1. Maana ya Kauli Mbiu – "Kazi na Utu Tunasonga Mbele"

Kauli hii ina sehemu tatu kuu:

1. Kazi – Inawakilisha juhudi, bidii na uzalishaji mali kwa maendeleo ya taifa.

2. Utu – Inahimiza maadili, mshikamano, heshima na haki za binadamu katika shughuli zote za kijamii na kiuchumi.

3. Tunasonga Mbele – Inasisitiza maendeleo endelevu yanayozingatia kazi na utu kama nguzo za mafanikio.

 


Kauli mbiu hii inatoa msingi imara kwa maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kisiasa kwa njia zifuatazo.

 

i. Maendeleo ya Kiuchumi kwa Kujenga Nchi ya Watu Wanaofanya Kazi

- Tanzania imekuwa ikiwekeza katika miradi mikubwa kama Mradi wa Umeme wa Maji wa Mwalimu Nyerere (JNHPP), Reli ya SGR, BRT, EACOP, na ujenzi wa barabara. 

- Miradi hii inaendana na sehemu ya “Kazi” kwani inahimiza watu kushiriki katika maendeleo ya taifa kupitia ajira na uwekezaji.

- Pia, inahimiza sekta binafsi na wajasiriamali kuchangia uchumi kwa kuendeleza biashara, kilimo, na viwanda.

 

ii. Uimarishaji wa Huduma za Jamii kwa Kujali Utu

- Serikali imewekeza katika elimu, afya na maji safi, ikiwa ni mwendelezo wa sehemu ya “Utu” ambapo maendeleo hayapaswi kuachwa mikononi mwa miradi ya kiuchumi pekee, bali pia yanapaswa kuheshimu na kuboresha hali ya maisha ya wananchi.

- Mfano mzuri ni uboreshaji wa elimu kupitia ujenzi wa madarasa zaidi ya 5,000 ya sayansi, huduma za afya kama ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Gairo kwa TZS 4.8 bilioni, na miradi ya maji inayoendelea kote nchini.

 

iii. Kazi na Utu katika Utawala Bora

- Serikali ya Awamu ya Sita imeonyesha dhana ya "Kazi na Utu" kwa kupambana na rushwa, kuongeza uwazi wa matumizi ya fedha za umma, na kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia.

- Rais Samia amesisitiza umuhimu wa majadiliano na maridhiano katika siasa, akijenga Tanzania inayoheshimu haki za binadamu huku ikisonga mbele kimaendeleo.

 

iv. Umoja na Amani Kama Msingi wa Utu

- Tanzania ni nchi inayotegemea amani kwa maendeleo yake. Kauli mbiu hii inahimiza mshikamano wa kitaifa, kuondoa ubaguzi, na kudumisha uzalendo.


3. Kauli Mbiu katika Mila na Desturi za Kitanzania

Katika mila na desturi za Kitanzania, kauli mbiu hii inahusiana na mambo yafuatayo:

 

i. Kazi kama Sehemu ya Utu katika Jamii

- Mila za Kitanzania zinatilia mkazo kazi kama njia ya kuleta heshima kwa mtu binafsi na jamii.

- Wahenga walisema: "Asiyefanya kazi, na asile", ikimaanisha kwamba mtu lazima achangie maendeleo ya jamii kupitia kazi.

 

ii. Utu Katika Mahusiano ya Jamii

- Desturi za Kitanzania zinahimiza mshikamano, heshima, na kusaidiana. Kauli mbiu hii inahimiza kuwa maendeleo hayapaswi kuja kwa gharama ya utu wa watu.

- Katika familia na jamii, utu umechukuliwa kuwa nguzo muhimu inayojenga mshikamano wa kitaifa.

 

iii. Kuendeleza Uzalendo na Mshikamano

- Kauli mbiu hii inatilia mkazo uzalendo kwa kufanya kazi kwa bidii na kuhakikisha tunasonga mbele kama taifa, huku tukidumisha heshima kwa kila mtu bila kujali kabila, dini, au hali ya kiuchumi.


"Kazi na Utu Tunasonga Mbele" – ni dira ya maendeleo yenye maana kubwa kwa taifa. Inaweka uwiano kati ya maendeleo ya kiuchumi na maadili ya kijamii, ikihimiza kazi kama msingi wa maendeleo huku ikidumisha utu kwa kila mtu.

 

Kauli hii imeweza kusawazisha juhudi za serikali katika kutekeleza miradi mikubwa, kutoa huduma bora kwa wananchi, na kudumisha mshikamano wa kitaifa. Pia, inaendana na mila na desturi za Kitanzania zinazohimiza mshikamano, heshima na uzalendo.

 

Watanzania wanapaswa kuitafsiri kauli mbiu hii kwa vitendo kwa kufanya kazi kwa bidii, lakini kwa kuzingatia utu, heshima na mshikamano wa kitaifa, ili kuhakikisha kwamba tunasonga mbele kama taifa lenye maadili na maendeleo endelevu.

Jumatano, 12 Machi 2025

RAIS SAMIA SULUHU HASSAN AHUTUBIA MKUTANO MKUU WA 39 WA ALAT JIJINI DODOMA

Dodoma, Tanzania – Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amehutubia viongozi pamoja na wageni mbalimbali waliokusanyika katika Mkutano Mkuu wa 39 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT). Mkutano huo umefanyika katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Centre, jijini Dodoma.  

Katika hotuba yake, Mhe. Rais Samia amesisitiza umuhimu wa serikali za mitaa katika kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa wananchi. Ameeleza kuwa serikali yake itaendelea kuimarisha ushirikiano na ALAT ili kuhakikisha kuwa changamoto zinazoikumba sekta ya utawala wa mitaa zinapatiwa suluhisho la kudumu.  


Aidha, Rais Samia amewataka viongozi wa serikali za mitaa kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa uadilifu, uwazi, na uwajibikaji ili kuwahudumia wananchi kwa ufanisi zaidi. Pia amewahimiza kutumia teknolojia za kisasa katika utoaji wa huduma ili kuongeza ufanisi na uwazi katika utawala wa mitaa.  

 

Mkutano huu wa ALAT umehudhuriwa na viongozi wa serikali, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, wabunge, madiwani, na wadau mbalimbali wa maendeleo. Pamoja na kujadili masuala ya utawala bora katika serikali za mitaa, mkutano huu pia umeweka mkakati wa kuimarisha utoaji wa huduma bora kwa wananchi katika ngazi za halmashauri nchini.  

 

Kwa upande wao, viongozi wa ALAT wamemshukuru Rais Samia kwa uongozi wake thabiti na dhamira yake ya kuimarisha utawala wa mitaa kwa maendeleo endelevu ya nchi.  

 

Mkutano huu wa 39 wa ALAT umeendelea kuwa jukwaa muhimu la kubadilishana mawazo, kutathmini mafanikio na changamoto, pamoja na kupanga mikakati ya kuimarisha utawala bora katika serikali za mitaa.

Jumanne, 25 Februari 2025

UJENZI WA UWANJA WA MPIRA WA MIGUU KMC KIJITONYAMA MWENGE WAKAMILIKA NA KUANZA KUTUMIKA

Kinondoni, Dar es Salaam – Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni imefanikiwa kukamilisha ujenzi wa Uwanja wa Mpira wa Miguu wa KMC, uliopo katika Kata ya Kijitonyama, Mwenge. Uwanja huu sasa umeanza kutumika rasmi, ikiwa ni hatua muhimu katika kuimarisha miundombinu ya michezo ndani ya manispaa hiyo.  

Leo, timu ya wataalamu na viongozi kutoka Manispaa ya Kinondoni ilifanya ziara ya kutembelea na kukagua uwanja huo, ambapo waliridhishwa na kiwango cha ujenzi na maandalizi yaliyofanywa kuhakikisha uwanja huo unakuwa wa viwango vya kisasa.  

Uwanja huu unatarajiwa kuwa chachu ya maendeleo ya michezo, hususan soka, kwa vijana wa Kinondoni na maeneo jirani, huku ukiwapa fursa ya kukuza vipaji na kushiriki mashindano mbalimbali.   

Manispaa ya Kinondoni inaendelea kuwekeza katika sekta ya michezo kama sehemu ya juhudi za kukuza afya, kuimarisha mshikamano wa jamii, na kuandaa vipaji vitakavyoiwakilisha Tanzania katika ngazi za kitaifa na kimataifa.  


Wananchi na wapenzi wa michezo wamehimizwa kuutumia uwanja huu ipasavyo ili kuhakikisha dhamira ya serikali ya kuimarisha michezo inatimia.

Jumatano, 19 Februari 2025

HISTORIA YA JIWE LA BISMARCK (BISMARCK ROCK) NA ZIWA VICTORIA NA MCHANGO WAKE KATIKA UCHUMI WA TANZANIA

  

Jiwe la Bismarck ni moja ya vivutio vikubwa vya utalii vilivyopo jijini Mwanza, Tanzania. Jiwe hili limekuwa kivutio cha pekee kutokana na muonekano wake wa kipekee, likiwa ni mwamba mkubwa unaoning’inia juu ya mawe mengine ndani ya Ziwa Victoria. Asili ya jina lake inahusiana na Chancellor wa Ujerumani, Otto von Bismarck, ambaye alikuwa kiongozi mashuhuri wakati wa ukoloni wa Wajerumani katika Afrika Mashariki. Inaaminika kwamba Wajerumani waliokuwa wakitawala eneo hilo mwishoni mwa karne ya 19 waliliita jiwe hilo kwa heshima yake.

 

Jiwe la Bismarck linajulikana kwa hadithi na simulizi mbalimbali za wenyeji wa Mwanza, ambapo baadhi yao huamini kuwa lina maana ya kiroho na lina historia ya kushikamana na tamaduni za kiasili za watu wa eneo hilo, hasa Wasukuma. Leo hii, jiwe hili ni moja ya vivutio vikubwa kwa watalii wa ndani na nje ya nchi, wakifika Mwanza kwa ajili ya kujionea mandhari yake ya kuvutia na kupiga picha.

Historia ya Ziwa Victoria  

Ziwa Victoria ni moja ya maziwa makubwa zaidi duniani na ndilo ziwa kubwa kabisa barani Afrika. Likiwa na eneo la takribani kilomita za mraba 68,800, ziwa hili linagawanyika kati ya nchi tatu: Tanzania (takribani 49% ya eneo lake), Uganda, na Kenya. Hili ni chanzo kikuu cha maji ya Mto Nile na limepewa jina na Mwingereza John Hanning Speke mnamo mwaka 1858, kwa heshima ya Malkia Victoria wa Uingereza.

 

Kabla ya kupewa jina la "Victoria," jamii zilizokuwa zikiishi kando ya ziwa hili zililiita kwa majina mbalimbali. Watu wa kabila la Wasukuma waliita ziwa hili "Nyanza," neno linalomaanisha "ziwa kubwa." Ziwa hili limekuwa kiini cha maisha ya watu wa Afrika Mashariki kwa karne nyingi, likihifadhi uhai wa jamii nyingi kupitia uvuvi, kilimo cha umwagiliaji, na usafirishaji.

Mchango wa Ziwa Victoria Katika Uchumi wa Tanzania  

Ziwa Victoria lina mchango mkubwa katika uchumi wa Tanzania kwa njia mbalimbali, zikiwemo.

 

1. Sekta ya Uvuvi  

Ziwa Victoria ni moja ya vyanzo vikubwa vya samaki, hasa sangara (Nile Perch) na sato (Tilapia), ambao ni bidhaa muhimu kwa soko la ndani na la kimataifa.

Sekta ya uvuvi imeajiri maelfu ya watu moja kwa moja na kwa njia zisizo za moja kwa moja kupitia biashara ya samaki, usindikaji, na usafirishaji wa mazao ya uvuvi.

Tanzania hupata mapato kupitia mauzo ya samaki nje ya nchi, hasa kwenye masoko ya Ulaya, Asia, na Amerika.

 

2. Utalii

Mbali na Jiwe la Bismarck, Ziwa Victoria linavutia watalii wanaopenda mandhari ya asili, michezo ya maji, na safari za uvuvi wa burudani.

Miji iliyo kandokando ya ziwa kama Mwanza, Bukoba, na Musoma imeendelea kuwa kitovu cha utalii kutokana na uzuri wa ziwa hili.

Hifadhi ya Taifa ya Rubondo, ambayo ipo ndani ya ziwa, ni kivutio kikubwa cha wanyamapori na watalii wengi kutoka ndani na nje ya Tanzania.

 

3. Usafiri na Usafirishaji  

Ziwa Victoria ni njia muhimu ya usafiri na biashara kati ya Tanzania, Uganda, na Kenya.

Meli za mizigo na abiria, kama vile MV Victoria na MV Mwanza Hapa Kazi Tu, huchangia katika maendeleo ya biashara za mpakani kwa kurahisisha usafirishaji wa bidhaa kati ya nchi hizi.

Usafiri wa majini umepunguza gharama za usafirishaji wa bidhaa kutoka sehemu moja hadi nyingine, hivyo kuongeza ufanisi wa biashara.

 

4. Kilimo cha Umwagiliaji  

Ziwa Victoria hutoa maji yanayotumika kwa shughuli za umwagiliaji, hasa katika mikoa ya Mwanza, Kagera, na Mara.

Wakulima wanaotegemea kilimo cha umwagiliaji kutokana na maji ya ziwa hili huzalisha mazao mengi kama vile mpunga, mboga, na matunda, hivyo kuchangia katika usalama wa chakula na uchumi wa taifa.

 

5. Ufugaji wa Samaki (Aquaculture) 

Katika miaka ya hivi karibuni, ufugaji wa samaki umeongezeka, ambapo mabwawa ya kisasa ya samaki yanajengwa pembezoni mwa ziwa ili kuongeza uzalishaji wa samaki.

Hii imeleta ajira kwa vijana na kusaidia kupunguza uvuvi haramu ambao umekuwa ukiharibu mazingira ya ziwa.

 

6. Uhifadhi wa Mazingira na Uendelevu wa Rasilimali za Maji 

Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na mashirika ya kimataifa imeanzisha programu za kulinda mazingira ya Ziwa Victoria dhidi ya uchafuzi wa maji, uvuvi haramu, na kuenea kwa magugu maji.

Hifadhi ya viumbe wa majini na uhifadhi wa vyanzo vya maji ni hatua muhimu katika kuhakikisha kuwa ziwa hili linaendelea kuwa chanzo cha uchumi kwa vizazi vijavyo.

Jiwe la Bismarck na Ziwa Victoria ni sehemu muhimu za historia, utalii, na maendeleo ya kiuchumi nchini Tanzania. Wakati Jiwe la Bismarck likiendelea kuwa kivutio cha kipekee kinachovutia watalii kutoka ndani na nje ya nchi, Ziwa Victoria linachangia kwa kiwango kikubwa katika uvuvi, utalii, usafirishaji, na uhifadhi wa mazingira. Ili kuendelea kunufaika na rasilimali hizi, juhudi za uhifadhi wa ziwa, udhibiti wa uvuvi haramu, na uwekezaji katika sekta ya utalii zinapaswa kuimarishwa ili kuchochea maendeleo endelevu ya kiuchumi nchini Tanzania.

Vijana wa Mwanza Waandika Historia Mpya ya Maendeleo

  Leo Februari 19,2026 ni siku ya kipekee kwa vijana wa Mwanza. Ni mwanzo wa enzi mpya—enzi ya matumaini, ubunifu na mafanikio. Uzinduzi wa ...