SERIKALI KUREJESHA ASILIMIA 20 YA MAPATO YA KODI YA ARDHI KWA HALMASHAURI
Serikali imetangaza kuwa asilimia 20 ya mapato yatokanayo na kodi ya ardhi zitarejeshwa kwa halmashauri husika mara baada ya kukamilika kwa Mkataba wa Makubaliano (MoU) kati ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Ofisi ya Rais – TAMISEMI. Hatua hii inalenga kuboresha usimamizi na ukusanyaji wa kodi hiyo katika maeneo mbalimbali nchini.
Kauli hiyo imetolewa bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Mtwara Mjini, Mheshimiwa Hassan Seleman Mtenga, aliyependa kufahamu lini Serikali itarejesha asilimia 20 ya mapato ya kodi ya ardhi kwa Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara Mikindani.
Dkt. Nchemba alieleza kuwa, kupitia Sheria ya Fedha ya mwaka 2023/24, Serikali ilifanya marekebisho ya Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa, Sura 290, ambayo inazitaka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Ofisi ya Rais – TAMISEMI kuingia Mkataba wa Makubaliano ya Ushirikiano (MoU). Mkataba huo utahakikisha kuna utaratibu mzuri wa usimamizi wa kodi ya pango la ardhi na urejeshaji wa asilimia 20 ya mapato hayo kwa halmashauri husika, ili kuziwezesha katika ufuatiliaji na ukusanyaji wa mapato hayo.
“Serikali iliweka utaratibu huu kwa lengo la kuongeza tija katika ukusanyaji wa mapato yatokanayo na pango la ardhi, pamoja na kuondoa changamoto zilizokuwa zinawakabili walipa kodi katika maeneo mbalimbali,” alifafanua Dkt. Nchemba.
Waziri huyo alihitimisha kwa kulihakikishia Bunge kuwa mara baada ya kukamilika kwa mkataba huo na kuwasilishwa Wizara ya Fedha, fedha hizo zitaanza kurejeshwa kwa halmashauri husika kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa.
Comments
Post a Comment