Alhamisi, 10 Julai 2025

Ushirikiano wa Tanzania na UNICEF Katika Sekta ya Maji - Serikali Yajizatiti Kuimarisha Huduma kwa Wananchi

Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) na Bi Elke Wisch, Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) nchini Tanzania

Na Mwandishi Wetu  Sisi Ni Tanzania

Katika jitihada za kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora ya maji kwa Watanzania, Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) ameendelea kuimarisha ushirikiano na mashirika ya kimataifa pamoja na nchi marafiki zinazounga mkono maendeleo ya sekta ya maji nchini.

Hivi karibuni, Mhe. Aweso amefanya mazungumzo muhimu na Bi Elke Wisch, Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) nchini Tanzania. Mazungumzo hayo yalilenga kuangazia umuhimu wa maji katika ustawi wa jamii, hasa katika nyanja za afya, elimu na ustawi wa wanawake na watoto.

Katika kikao hicho, Waziri Aweso amepongeza mchango wa UNICEF kwa kuwa mdau muhimu katika utekelezaji wa miradi ya maji, usafi wa mazingira, na mabadiliko ya tabianchi. “UNICEF imekuwa mshirika wa karibu kwa muda mrefu. Tunatambua na kuthamini mchango wake mkubwa katika kuinua maisha ya Watanzania kupitia miradi ya kimkakati ya maji,” alisema Waziri Aweso.

Kwa upande wake, Bi Elke Wisch ameahidi kuendeleza ushirikiano na Serikali ya Tanzania kwa kuzingatia vipaumbele vya kitaifa katika sekta ya maji, hasa maeneo yenye uhitaji mkubwa na yenye changamoto za kiikolojia.

Mazungumzo hayo pia yalihudhuriwa na Bi Gemma Querol, Mkurugenzi wa masuala ya maji wa UNICEF, ambaye alieleza kuwa shirika hilo linaendelea kujipanga kusaidia Tanzania katika kufikia malengo ya maendeleo endelevu (SDGs), hasa lengo la 6 linalolenga upatikanaji wa maji safi na usafi wa mazingira kwa wote.

Ushirikiano wa Tanzania na Ujerumani Kwenye Sekta ya Maji

Katika tukio lingine, Waziri Aweso alikutana na Naibu Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania, Bw. Manuel Muller, pamoja na ujumbe kutoka KfW, benki ya maendeleo ya Ujerumani. Mazungumzo yao yalihusu ushirikiano wa muda mrefu baina ya Tanzania na Ujerumani katika utekelezaji wa miradi ya maji nchini.

Bw. Muller alieleza kuwa miradi iliyotekelezwa kupitia ushirikiano huo imeleta manufaa makubwa kwa jamii na kueleza matumaini yake kuwa miradi inayoendelea nayo itazaa matokeo chanya.

Kwa upande wa Serikali ya Tanzania, Waziri Aweso ameahidi kuendeleza ushirikiano huo na kuhakikisha kuwa miradi yote inakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyokubalika. “Tuna dhamira ya dhati ya kutekeleza miradi hii kwa ufanisi mkubwa. Lengo letu ni kufikia asilimia 85 ya upatikanaji wa huduma ya maji vijijini na asilimia 95 mijini ifikapo 2030,” alisisitiza Waziri Aweso.

Maoni 1 :

  1. Kazi nzuri sana, sasa maji yanamwagika mwaaa mwaaa kila kona ya tanzania

    JibuFuta

VIJANA WAVUNA DHAHABU YA SAMAKI ZIWA VICTORIA: UWEKEZAJI WA VIZIMBA NA UMEME WA JUA CHINI YA UFADHIRI WA TADB WAFUNGUA MILANGO YA AJIRA NA UTAJIRI MPYA TANZANIA

Ufugaji wa samaki kwa kutumia vizimba ndani ya Ziwa Victoria umeanza kuwa nguzo muhimu ya kuimarisha uchumi wa vijana na kuchangia usalama w...