 |
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Cyprus leo zimesaini hati za makubaliano (MoU) |
Dar es Salaam, 9 Julai 2025 – Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Cyprus leo zimesaini hati za makubaliano (MoU) za kushirikiana katika mashauriano ya kisiasa na usafiri wa majini, hatua inayolenga kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia baina ya nchi hizo mbili.
Hati hizo zimesainiwa wakati wa ziara ya kihistoria ya siku tatu nchini Tanzania ya Mhe Dkt. Constantinos Kombos, Waziri wa Mambo ya Nje wa Cyprus. Akifungua mkutano huo, mwenyeji wa mgeni huyo Balozi Mahmoud Thabit Kombo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, alisema ziara hii ni muhimu kwa sasa kwani uhusiano wetu umeamshwa na fursa mbalimbali za kiuchumi baina ya nchi zetu.
Akizungumzia kuhusu makubaliano yaliyosainiwa, Mhe. Kombo alisema ni matumaini ya Serikali kuwa makubaliano hayo yataleta chachu ya kuimarisha ushirikiano katika sekta mbalimbali – ikiwemo utalii, kilimo, uchimbaji na utafiti wa madini, uchumi wa buluu, vyombo vya usafiri ikiwemo meli za biashara, soko la ajira, nishati mbadala na kuwezesha uwekezaji unaoongeza thamani.
Hatua hii itaziwezesha nchi hizi kuleta maendeleo endelevu kwa wananchi wake huku ikiimarisha nguvu kazi na pato la Taifa.
“ Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye uchumi unaokuwa kwa kasi zaidi Barani Afrika, na inatarajiwa kufikia ukuaji wa uchumi wa asilimia sita, mwishoni mwa mwaka huu kwa mujibu wa IMF. Mafanikio haya yanatokana na amani na utulivu uliyopo nchini pamoja na mazingira mazuri ya uwekezaji nchini".
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Cyprus Mhe. Dkt Kombos, ameipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa hatua chanya za ukuaji uchumi na kuimarisha uhusiano wa Kimataifa, kwani umesaidia kunufaisha Watanzania na kufungua milango ya fursa kwa mataifa mengine.
Mhe. Kombos amesema Serikali ya Cyprus itaendelea kukuza ushirikiano wake na Tanzania uliodumu kwa zaidi ya miaka 40, kwa kuangalia fursa mpya za ushirikiano zinazozingatia mahitaji ya pande zote na dira za maendeleo endelevu za mataifa hayo.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni