Dodoma, Julai 2025 — Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imetangaza rasmi kuwa Uchaguzi Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania utafanyika Jumatano, tarehe 29 Oktoba 2025, kwa mujibu wa mamlaka iliyopewa chini ya Ibara ya 74(6) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977, na kwa kuzingatia Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 pamoja na Kanuni za Uchaguzi za mwaka 2020.
1. Uhalali wa Tangazo hilo Kikatiba
Kwa mujibu wa Ibara ya 74(6)(e) ya Katiba, Tume ya Uchaguzi ina jukumu la kutangaza na kusimamia uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani. Kutangaza tarehe ya uchaguzi mkuu ni sehemu ya utekelezaji wa wajibu huo wa kikatiba, kwa lengo la kutoa mwongozo rasmi wa mchakato wa kidemokrasia.
2. Uteuzi wa Wagombea: Taratibu na Ratiba
Jaji wa Rufaa Jacob Mwambegele, Mwenyekiti wa INEC, ametangaza kuwa utoaji wa fomu za uteuzi kwa wagombea wa nafasi ya Rais na Makamu wa Rais utaanza Agosti 9 hadi 27, 2025. Tarehe 27 Agosti 2025 itatumika kama siku rasmi ya uteuzi wa wagombea kwa nafasi zote tatu: Rais, Wabunge, na Madiwani.
Hii inatekeleza matakwa ya Sheria ya Uchaguzi wa Rais na Wabunge, Sura ya 343, inayotaka mchakato wa uteuzi ufanyike kwa uwazi na kufuata kalenda ya uchaguzi.
3. Kampeni za Kisiasa: Usawa wa Kikatiba na Kidemokrasia
Kwa mujibu wa Kanuni ya 42 ya Kanuni za Uchaguzi (2020), kipindi cha kampeni kinatakiwa kuwa huru, haki, na kinachotoa nafasi sawa kwa vyama vyote. INEC imetangaza kuwa kampeni zitaanza Agosti 28 hadi Oktoba 28, 2025kwa Tanzania Bara, na Agosti 28 hadi Oktoba 27 kwa Zanzibar ili kuruhusu maandalizi ya upigaji kura ya mapema, hatua inayozingatia mazingira ya kiutawala ya Muungano kwa mujibu wa Ibara ya 2 na 3 ya Katiba ya JMT.
4. Maslahi Mapana ya Taifa: Demokrasia, Amani na Ushirikishwaji
Tangazo hili linatoa fursa kwa Watanzania wote kujipanga kushiriki uchaguzi kwa amani, kwa mujibu wa haki yao ya msingi ya kushiriki katika uongozi wa taifa lao kama ilivyoainishwa katika Ibara ya 21(1) ya Katiba, inayosema:
"Kila raia wa Tanzania anayo haki ya kushiriki katika shughuli za utawala wa nchi, ama moja kwa moja au kwa kupitia wawakilishi waliowachagua kwa hiari yao."
Hatua ya INEC kutangaza ratiba mapema ni kielelezo cha uwazi na maandalizi ya kitaasisi kuelekea uchaguzi huru, wa haki na unaozingatia misingi ya katiba. Ni wajibu wa vyama vya siasa, wagombea, na wananchi wote kuhakikisha wanashiriki kwa amani, wanatii sheria na kutoa kipaumbele kwa maslahi ya taifa kuliko maslahi binafsi au ya kisiasa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni