WANANCHI JIJINI DODOMA WAMPONGEZI RAIS SAMIA, WAHIMIZA ELIMU KUPINGA DAWA ZA KULEVYA IENEZWE NCHI NZIMA
Baadhi ya wananchi waliohudhuria fainali ya mpira wa miguu iliyofanyika katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Mtakatifu John, jijini Dodoma, wamepongeza jitihada zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kupitia Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), kwa kuendelea kuwekeza katika kinga na tiba ya waathirika wa dawa za kulevya pamoja na utoaji wa elimu endelevu kwa vijana.
Michuano hiyo ya mpira wa miguu, ambayo imeandaliwa na Mamlaka ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya DCEA, imekuwa sehemu ya jukwaa la kijamii kuhamasisha mapambano dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya miongoni mwa vijana. Katika mchezo wa fainali uliovutia mamia ya mashabiki, timu ya Wagoloko FC iliibuka mshindi kwa kuifunga timu ya Mwaise FC mabao 2–0.
Akizungumza wakati wa fainali hiyo, Mwalukasi Sidi Jonjolo, mmoja wa wananchi waliokuwepo uwanjani, alitoa wito kwa serikali kuhakikisha elimu kuhusu madhara ya dawa za kulevya inasambazwa zaidi katika kanda zote nchini. Alisisitiza kuwa elimu hiyo ifike kuanzia shule za msingi hadi vyuo vikuu ili kuokoa kizazi cha sasa na kijacho dhidi ya mtego wa uraibu wa dawa hizo.
Aidha, Jonjolo alisisitiza umuhimu wa michezo katika kujenga afya ya vijana, kuwaepusha na matumizi ya dawa za kulevya na kuwaandaa kuwa raia wenye mchango chanya katika taifa. “Michezo ni njia bora ya kuwafanya vijana wajishughulishe, waepuke vishawishi na wakue kimaadili. Tunaomba michezo iendelee kuungwa mkono,” alisema.
Wananchi hao walihitimisha kwa kutoa pongezi kwa Rais Samia kwa dhamira yake ya dhati katika kutetea afya ya vijana wa Tanzania, kupitia mikakati ya kinga, tiba na elimu. Waliomba DCEA kuendeleza mashindano kama hayo katika maeneo mengine ya nchi ili kuongeza hamasa ya mapambano dhidi ya dawa za kulevya kwa njia chanya, jumuishi na inayogusa maisha ya wananchi moja kwa moja.
Kauli mbiu: "Wekeza kwenye Kinga na Tiba dhidi ya dawa za kulevya"
Comments
Post a Comment