WANANCHI WA KIHURIO WAELIMISHWA KUHUSU HUDUMA SALAMA ZA KIFEDHA.
Same, Kilimanjaro – Wananchi wa Kata ya Kihurio, wilayani Same, mkoani Kilimanjaro, wametakiwa kuhakikisha wanatumia huduma za taasisi za fedha zilizosajiliwa na zenye leseni kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ili kuepuka matatizo yanayosababishwa na taasisi zisizo rasmi.
Rai hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa Kata ya Kihurio, Bw. Rafaeli Tomasi, alipokutana na wataalamu kutoka Wizara ya Fedha waliokuwa katika ziara ya kutoa elimu ya fedha kwa wananchi wa eneo hilo.
Akizungumza katika mkutano huo, Bw. Tomasi alisema kumekuwepo na baadhi ya taasisi zinazotoa mikopo kwa wananchi bila kuzingatia sheria, hali inayosababisha malalamiko mengi, ikiwa ni pamoja na wananchi kupoteza mali zao walizoweka kama dhamana.
"Tumesisitiza kuwa watoa huduma za kifedha na taasisi zinazotoa mikopo wilayani hapa wanapaswa kuhakikisha huduma zao haziwaletei madhara wananchi. Serikali haitasita kuchukua hatua za kisheria kwa yeyote atakayekiuka kanuni za fedha na mikopo," alisisitiza Bw. Tomasi.
Elimu ya Fedha Kuimarisha Uelewa wa Wananchi
Katika mafunzo hayo, wananchi walifundishwa kuhusu haki na wajibu wao wanapochukua mikopo, namna ya kutathmini viwango vya riba, na umuhimu wa kusoma mikataba kabla ya kukubali masharti ya mikopo.
Bw. Tomasi alieleza kuwa elimu hiyo itawasaidia wananchi kuepuka mikopo yenye masharti magumu au yenye athari mbaya kwa uchumi wao. Alitoa pongezi kwa Wizara ya Fedha kwa kuleta elimu hiyo hadi katika ngazi ya kata na vijiji, akisisitiza kuwa hatua hiyo itawanufaisha wananchi wengi ambao mara nyingi hawapati fursa ya kujifunza masuala ya fedha.
"Tunampongeza Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, kwa kuhakikisha elimu ya fedha inawafikia wananchi wote na kuwawezesha kukabiliana na changamoto za kiuchumi," alisema Bw. Tomasi.
Kwa upande wake, Afisa Usimamizi wa Fedha kutoka Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha katika Wizara ya Fedha, Bw. Stanley Kibakaya, alisema kuwa mpango huu wa kutoa elimu ya fedha ni endelevu na unalenga kuwawezesha wananchi kufahamu fursa zilizopo katika sekta ya fedha na kuzitumia kwa usahihi.
"Hatua hii ni sehemu ya dhamira ya Serikali kuhakikisha usawa wa kiuchumi kwa makundi yote ya jamii, ikiwa ni pamoja na wanawake, vijana, walemavu na wazee. Tunataka wananchi wote wawe na uelewa wa kutosha kuhusu huduma za kifedha ili waweze kufanya maamuzi sahihi," alisema Bw. Kibakaya.
Mpango huu wa elimu ya fedha ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha wa mwaka 2020/21 – 2029/30, ambao unalenga kuhakikisha sekta ya fedha inakua kwa kasi na kuchangia maendeleo endelevu ya taifa.
Wananchi wa Kihurio wamefurahishwa na elimu hiyo na kuahidi kuwa waangalifu wanapotumia huduma za kifedha, ili kuepuka matatizo yanayotokana na taasisi zisizofuata sheria.
Ni dhamira ya kweli ya muheshimiwa Rais katika kuwasaidia Wananchi wake Hasa wenye kipato Cha Chini kupata msaada Wa Kisheria.
ReplyDelete#MSLAC #Katibanasheria #SSH #CCM #KaziIendelee #Nchiyangukwanza #SisiniTanzania #matokeochanya